Mafunzo 5 Katika Filamu ya "Soul Surfer"
Akiwa na umri wa miaka 13, Bethany anakumbwa na janga kubwa baada ya kung’atwa na papa, jambo lililosababisha kupoteza mkono wake wa kushoto. Kama umewahi kushuhudia mchezo huu, utagundua ni mchezo unaohitaji ujuzi, nguvu na mazoezi ya hali ya juu. Unahusisha matumizi ya karibu viungo vyote vya mwili — miguu kwa kusimama na kuteleza, na mikono kwa kudhibiti usawa (balance).
Soul Surfer ni filamu ya mwaka 2011 inayosimulia hadithi ya kweli ya msichana huyo Bethany Hamilton, ambaye alikuwa na mapenzi makubwa kwa mchezo wa kuteleza juu ya mawimbi baharini (surfing).
Sasa fikiria mtu anayeweza kuendelea kucheza mchezo huo akiwa amepungukiwa mkono mmoja. Baada ya kunusurika kifo, Bethany anafanya uamuzi mgumu wa kurudi baharini. Hajui kwamba safari hiyo mpya itamhitaji nguvu, imani, na kujitolea zaidi kuliko hapo awali. Kwa ulemavu aliokuwa nao, mambo mengi aliyoyafanya kwa urahisi zamani sasa yanakuwa changamoto kubwa.
Kwa juhudi binafsi pamoja na msaada wa familia, marafiki na jamii yake, Bethany anarudi katika ubora wake na anakuwa chanzo cha matumaini kwa mamilioni ya watu wenye ulemavu duniani.
Leo, Bethany ameendelea kuchukulia mchezo wa surfing kama taaluma yake, huku akitumia hadithi yake kuwahamasisha watu kutokata tamaa licha ya changamoto wanazokutana nazo maishani.
Filamu hii imeongozwa na Sean McNamara ikiwa ni kumbukumbu ya kitabu ( yaani autobiography) Soul Surfer: A True Story of Faith, Family, and Fighting to Get Back on the Board kilichoandikwa na Bethany Hamilton mwenyewe pamoja na Sheryl Berk na Rick Bundschuh.
Na haya ndiyo mafuzo 5 unayoweza kujifunza kutoka katika filamu hii ya Soul Surfer.
- Gundua kusudi lako na ufanye unachokipenda.
Baada ya tukio la kushambuliwa na papa, Bethany alibakia na mkono mmoja. Kwa mtu mwingine, hiyo ingekuwa sababu ya kuachana kabisa na ndoto zake. Labda angejificha, au kuishi kwa huzuni na kujilaumu maisha yake yote. Lakini Bethany anatufundisha kuwa—penye nia, pana njia. Kwasababu aliupenda kwa dhati mchezo wa kuteleza kwenye mawimbi, hakukubali kuachana nao.
Alichagua kurudi, kujifunza njia mpya, na kuendelea kufanya kile alichokipenda kwa moyo wake wote. Na hapo ndipo alipoanza kugundua kusudi lake. Kusudi ambalo halikuishia tu kwenye ushindani, bali katika kuhamasisha wengine waliokata tamaa.
- Kuwa mvumilivu na mstahimilivu unapokutana na changamoto.
Kamwe usikate tamaa, baada ya Bethany kushambuliwa na papa maisha yake yalibadilika, hakuweza kufanya vitu alivyoweza kufanya zamani kwa ukawaida. Sasa ilimbidi atumie miguu na mikono kwa kitu ambacho angeweza kufanya kwa mikono miwili tu. Hata kurejea majini haikuwa haraka, ilibidi azoee na kukubaliana na hali aliyokuwa nayo kwanza.
Hii ilikuwa ni changamoto kama changamoto nyingine ambazo mtu hukutana nazo maishani; kufeli shule, kufukuzwa kazi, kupotelewa na kitu cha thamani (mali labda). Changamoto zote hizo zinatufanya tukwame wakati fulani lakini tukiwa wavumilivu na wastahimilivu tutapata njia nyingine za kukabiliana na changamoto zetu na kuzitumia kama fursa.
- Jenga Imani isiyotikisika.
Mara nyingi tumeshindwa kutimiza makusudio yetu kwa kushindwa kuwa na imani katika kile tunachokifanya. Kuna msemo wa tangazo unaosema “wale wanaofikiri kuwa wana uwezo uliopitiliza kubaidilisha dunia, hatimaye hufanya hivyo”.
Bethany ni kielelezo halisi cha Imani hiyo, imempa nguvu katika jambo alilokusudia kufanya na akafanikiwa. Kwenye mashindano Bethany hakutaka kupendelewa kwasababu ana mkono mmoja, aliamini katika uwezo wake wa kuteleza kwenye mawimbi. Kabla ya hapo Bethany alitaka kujua kama inawezekana kurudi majini na kwasababu aliamini hiyo ndiyo ilikuwa nguvu yake ya kumsukuma wakati wa dhiki.
- Guswa na changamoto za wengine.
Baada ya Bethany kushindwa kwenye mashindano na kwenda kwenye safari ya kidini huko Thailand, Phuket kwenye watu waliopatwa na janga la Tsunami. Bethany aliguswa na changamoto yao ya kuwa na hofu iliyowatawala na kuogopa kusogelea fukwe kutokana na kile ilichowafanyia.
Kwa kupenda kucheza kwenye maji na kuteleza kwenye mawimbi, Bethany aliwatoa hofu watu wa huko kwa yeye kuwa wakwanza kusogelea bahari kisha watoto.
Pia kutokana na ujasiri wake wa kutaka kurejea kwenye mchezo wa kuteleza na mawimbi baada tu ya kupoteza mkono wake wa kushoto kuliwahamasisha na kuwapa moyo watu wenye changamoto zinazofanana na yeye. Aliporudi tu kutoka Thailand alikutana na mafurushi ya barua watu wakimshukuru kwa ujasiri aliowajaza ndani yao. Hii inatufundisha uzoefu na changamoto mbalimbali tunazopitia kwenye maisha zinaweza kuwa chanzo cha kuwahamasisha wengine.
- Jifunze kuwa na mtazamo chanya wakati wote.
Hakuna anaeweza kuzuia jambo la ghafla lisimkute. Katika mazingira ya ajali, kupoteza mtu wa karibu, biashara kuanguka, magonjwa, changamoto za kimasomo n.k. Vyote hivyo humfanya mtu aangalie maisha kwa jicho la tofauti kabisa akitafuta njia za kujihami na mda mwengine kupoteza dira kabisa. Bethany anatufundisha tuwe na mtazamo chanya katika kila hali inayotukuta, hata kama ni ya kuhuzunisha tuangalie ni nini tunaweza fanya ambacho kina manufaa kuliko kuendelea kuwa kwenye maumivu au majonzi. Bethany baada ya kupoteza mkono wake wa kushoto aliamua kuwa na mtazamo chanya, hatimaye aliweza kurejea kwenye mchezo alioupenda.
Baada ya kusoma mafunzo haya yatokanayo na filamu hii, ni funzo gani limekugusa zaidi? Hebu tujadili kwenye sehemu ya maoni! Na kama kuna filamu nyingine ungependa tuitupie jicho hapa Purpose Reels, tuambie kwenye maoni pia!
Hii ni safari yetu ya kuendelea kuchambua filamu zenye maana kubwa na kujifunza kutoka kwa wahusika na hadithi zao.